{ Kama nimesema vibaya toa ushahidi wa neno baya
Bali kama nimesema vema kwanini wanipiga? } *2
[ s ] Pilato alimhukumu Yesu, ingawa hakuona kosa kwake
Aliwaogopa Wayahudi, na kubembeleza urafiki wa Kaisari
Ndugu yangu tafakari kwa makini, mamlaka ulopewa na wenzio
Unayatumia ipasavyo au waumiza wenzako kama Pilato
Askari usalama wa raia, acheni kuwadhulumu raia,
Na kusingizia watu kesi, mnasababisha uvunjaji wa sheria
Mahakimu na mabingwa wa sheria, haifai kuipotosha sheria,
Maskini wajane na yatima mnawanyang`anya haki zao hukumuni
Waganga wakunga na wauguzi, tibuni bila kudai zawadi,
Watu masikini na yatima wanahangaika vitandani hadi kufa
Wanandoa tunzeni ahadi zenu, kupendana katika shida na raha,
Pia kuwalea wana katika njia impasayo Mkristo
Utoaji wa mimba bila sababu, na kutupa watoto majalalani,
Ni kutoujali utu wa mtu, na kuwahukumu kifo wasio na kosa
Dunia yetu inawaka moto, amani yetu imeshatoweka,
Vita vyatawala kila kona kisa ni tamaa ya mali na madaraka